Pages

Subscribe:

Ads 468x60px

Friday, 27 November 2009

BILA USAFI KIPINDUPINDU KITATUMALIZA

WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaam wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari katika suala la usafi ili kusaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu.

Hatua hiyo imekuja baada ya idadi ya wagonjwa wa kipindupindu kuongezeka kutoka tisa hadi 38 ambao wamelazwa katika hospitali za Manispaa za Wilaya ya Temeke, Ilala, na Kinondoni.

Akitoa taarifa za ugonjwa huo Dar es Salaam jana Kaimu Mganga Mkuu wa jiji Dkt. Hawa Kawawa alisema wagonjwa 19 wametoka Wilaya ya Ilala na 11 Temeke.

"Mpaka sasa tuna wagonjwa 38 tumewapokea juzi asubuhi na wa zamani wanane, wengi wao wametoka maeneo ya Pugu, Vingunguti, Kiwalani, Segerea, Kiwalani, Kipawa , Ukonga, Ilala, Tabata, Majoe, Yombo Vituka na Kinyerezi ambao wanaendelea kupata matibabu," alisema Dkt. Kawawa

Dkt Kawawa alisema ukaguzi wa maeneo ya biashara unaendelea kufanywa katika manispaa zote ili kudhibiti maambukizi zaidi ya ugonjwa huo, na dawa za kukabiliana na ugonjwa huo zimesambazwa katika zahanati na hospitali tatu za wilaya.

"Tunaishukuru serikali kwa kutoa dawa hasa dripu kwani tumejitahidi kuwatibu wagonjwa kadri inavyowezekana ndio maana hakuna kifo hata kimoja, lakini wananchi wnatakiwa kuchukua tahadhari zaidi ili kumaliza tatizo hilo," aliongeza.

Aidha amewataka wananchi kuzingatia usafi, wafunike vyakula pindi wanapomaliza kupika, kunawa mikono kabla ya kula na wanapotoka chooni, wachemshe maji ya kunywa na kila wanapopata dalili za kipindupindu, ambazo ni kuharisha maji yenye rangi ya mchele na kutapika wawahi hospitali ili kupatiwa matibabu.

0 comments: