Pages

Subscribe:

Ads 468x60px

Wednesday, 19 May 2010

Watoto waunguzwa nyayo kukomesha kuzurura !

WATOTO wawili wakazi wa Mtaa wa Bangwe Manispaa ya Kigoma-Ujiji, mkoani Kigoma wamenusurika kifo baada ya mama yao mzazi kuwachoma moto katika nyayo za miguu kwa tuhuma za uzururaji.

Katika tukio hilo lililotokea Jumapili, mama aliyetambulika kwa jina la Fatuma Sambeki (25) aliwachoma moto nyayo watoto wake wawili akiwatuhumu kuzurura hadi usiku.

Watoto waliochomwa moto ni Ismail Swed (5) na Abedi Swed (3) ambao inadaiwa siku ya tukio walikwenda kutembea kwa bibi yao mzaa mama na kurejea saa mbili usiku nyumbani kwao.

Walipofika mama huyo aliwafokea kwa kitendo hicho, akawapiga na kuwachoma moto kwenye nyayo kwa kutumia banio la mkaa lililopashwa moto.

Bw. Kala Ntaruha shuhuda ambaye ni mjumbe wa Serikali ya Mtaa alisema kuwa baada ya kusikia kelele za watoto hao alifika kuona nini kinawasibu, ndipo alipokuta mtoto mmoja akiwa anaugulia maumivu ya madonda ya moto huo wakati mwenzake akiwa amefichwa chumbani na mama huyo.

Mjumbe huyo alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo waliripoti katika Kituo cha Polisi mjini Kigoma na mtuhumiwa akatiwa mbaroni jana.

Akizungumzia tukio hilo mume wa mtuhumiwa, Bw. Swed Abed (32) alisema kuwa siku ya tukio alikuwa katika shughuli zake za uvuvi ndipo alipata habari za kitendo hicho.

Bw. Abed aliongeza kuwa mkewe amekuwa akifanya matukio mengi ya ajabu, yakiwamo ya kuwapiga watoto hao na aliwahi kuchoma moto nyumba yao kabla ya majirani kukusanyika na kufanikiwa kuuzima.

Alisema kuwa mkewe amekuwa na matatizo ya kuchanganyikiwa, hasa kwa wakati kama huu ambao ni mjamzito na mara nyingine matatizo hayo humfika mwisho wa mwezi.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, ACP George Mayunga alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kuwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamni wakati wowote mara baada ya upelelezi kukamilika.

Hili ni tukio la pili la ukatili dhidi ya watoto mkoani Kigoma, baada ya mama mmoja wilayani Kibondo kukamatwa kwa tuhuma za kumchinja mtoto wake aliyekuwa anasadikiwa kuwa mlemavu wa viungo na akili na kesi ipo mahakamani.
Chanzo gazeti la majira.

0 comments: