Pages

Subscribe:

Ads 468x60px

Monday, 15 August 2011

Tujikumbushe kidogo historia ya Mtwa Mkwawa,alikufaje? na wapi?

Mkwawa aliongoza mapigano dhidi ya wakoloni wa Kijerumani kwa karibu miaka minane. Mwaka 1891 majeshi yake yalifanikiwa kumuua kamanda wa majeshi ya kikoloni von Zelewski, na wanaosafiri Iringa wanaweza kuliona kaburi lake pembeni ya barabara ya Dar es salaam kwenda Iringa, kama kilometa 40 kutoka Iringa mjini. Wenyeji wa Iringa wanalitambua kaburi hilo kama la Nyundo.

Lakini Wajerumani waliongeza nguvu na kuelekea mwisho wa utawala wa Mkwawa. Wajerumani walijenga kambi katika eneo la sasa la Tosamanganga, mwinuko wa Lugulu, na kutumia mizinga kutupa mabomu kwenye ngome ya Lipuli - yaani Kalenga.

Hatimaye walifanikiwa na hivyo kumfanya Mtwa Mkwawa atoroke, akawa amepoteza ngome yake, akaendesha vita vya msituni huku akiwapatia askari wa Kijerumani hasara kubwa sana katika mtindo huu wa kupigana kwa kushitukiza.

Aidha wananchi walimpenda sana Mkwawa kwa hiyo haikuwa rahisi kutambua yuko wapi, ingawa kuna maelezo kutoka kwa wahifadhi katika Makumbusho ya Mkwawa pale Kalenga, kuwa kuna mmoja wa ndugu zake waliobadilika kuwa Wakristo alitumika kumpeleleza, ingawa yeye mwenyewe alikataa kuwa hakuwa kibaraka wa Wazungu, na akaamua kwenda kukaa mbali kidogo na Kalenga. Alifia huko na kumbukumbu yake iko huko.

Lakini Wajerumani, kutokana na baadhi ya maandishi, waliendela kumtafuta na hatimaye kufanikiwa kumzingira. Lakini yeye alifanikiwa kutoroka na kuelekea eneo linaloitwa Mlambalasi, akiwa na walinzi wake wawili.

Lakini alishatambua kuwa uwezo wake wa kuendelea na vita umekwisha kwani walikuwa wamezingirwa na askari wake wengi kuuawa.

Ndipo alipokuwa hapo Mlambalasi, aliamuru askari wake wakoke moto mkubwa wa kuni na kumtuma mwingine akaongeze kuni. Lakini wale askari walitambua kuwa hiyo ilikuwa ni ishara ya kutaka kujiua.

Yule askari aliyetumwa, kwa maelezo niliyoyapata, alipofika mbali kidogo, alisikia milio miwili ya bunduki iliyofyatuliwa. Alihisi mlio wa kwanza ulikuwa wa Mkwawa kumuua askari mlinzi aliyebaki, na wa pili, ulikuwa wa kujiua mwenyewe. Aliporudi alikuta Mkwawa amekufa.

Hapa kuna maelezo yanayotatanisha. Baadhi wanasema kwa kukataa asitambuliwe na wakoloni baada ya kifo chake, alipojiua alikaa katika hali ya kuangukia kwenye moto ili aungue na asitambulike. Na kuwa askari wa kijerumani aliyefika alipoonyeshwa mwili wa Mtwa Mkwawa aliamua kumpiga risasi kichwani.

Lakini maelezo mengine ambayo ndiyo yanayofahamika zaidi yanasema kuwa Mtwa Mkwawa alipokufa hakuangukia motoni. Hata hivyo utafiti wangu wa intaneti nilifikishwa mahali penye orodha ya picha zinazomhusu Mtwa Mkwawa, moja ni ya fuvu, lakini ya pili ni ya mwili wa mtu ambaye mgongoni anaonekana kuwa na jeraha kubwa sana linalofanana na kuungua moto.

Sikuwa na namna ya kuthibitisha kuwa mwili huo ndio wa Mtwa Mkwawa uliongua moto baada ya kujiua? Na kwa nini uliwekwa pamoja na picha ya fuvu lake na mnara wa mahali alipojiua.

Ukifika Kalenga na kwenye makumbusho yake ukaulizia eneo la Mlambalasi ni wazi utapata watu wa kukuongoza na hadi kwenye kaburi na mnara mahali alipojiua. Mnara huu ni kumbukumbu ya ushujaa wake. Na kama tulivyowahi kusema awali kuwa taarifa za Mtwa Mkwawa zinahitaji kufanyiwa utafiti wa kina na kuwatafuta wataalamu wa Historia na mambo ya kale kutusaidia kufahamu nini hasa kilitokea.

Aidha kuna familia za ukoo wa Mkwawa kule Kalenga ambazo zinatunza historia na mengine yanayomhusu Mkwawa. Huenda hao wanaweza kutusaidia kutoa taarifa.Eneo la Kalenga pamoja na kuwa na historia kubwa bado ni sehemu ya kivutio cha utalii ambacho kama kitatangazwa hapana shaka kitafungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo na pato kwa nchi.
credit to mwananchi.

3 comments:

Rachel Siwa said...

Ahsante da'Edna kwa kumbukumbu ya Mkwawa.

Simon Kitururu said...

Asante kwa shule!

Kapoma said...

DADA UNA KUKUMBU NZURI KEEP IT UP