TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 19, 2013 Chama Cha Mapinduzi kilifanya
kikao cha siku moja na wabunge wanaotokana na CCM, kikao hicho kilifanyika
mjini Dodoma
ambapo pamoja na viongozi wengine wa juu wa CCM kikao hicho kilihudhuriwa pia
na Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la
wabunge wa CCM na viongozi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM
ambaye pia ni Rais na mtekelezaji mkuu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM
kubadilishana uzoefu wa namna ilani ilivyotekelezwa hasa kwenye majimbo kwa
kipindi cha nusu ya muhula wa miaka mitano. Baada ya kubadilishana mawazo
uliwekwa mwelekeo wa namna bora ya kutekeleza ilani na ahadi mbalimbali kwa
kipindi kilichobaki.
Kwahiyo kwa kifupi lengo la kikao
hicho ilikuwa ni kutathimini utekelezaji wa ilani majimboni na kuangalia namna
bora ya kuweka msukumo mpya na mkubwa zaidi kwa kipindi kilichobaki cha
utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa 2010/2015, lengo likiwa kuhakikisha
ilani na ahadi za CCM na wagombea wake zinatekelezwa kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo baada ya semina hiyo
baadhi ya vyombo vya habari vimenukuu kauli inayodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa CCM Dr. Jakaya
Kikwete kuwa ameruhusu wanaokusudia kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais wa 2015
kufanya kampeni.
CCM imesikitishwa na nukuu hiyo ya
kupotosha ukweli wa kilichojadiliwa na hivyo tumelazimika kutoa ukweli wa
kilichojiri na kujadiliwa. Ni kweli kuwa mjadala juu ya watu mbalimbali
wanaotajwa au wanaojitaja kuwa na nia ya kugombea nafasi mbalimbali hasa udiwani,
ubunge na Urais ulikuwepo na ulikuwa mkali.
Hata hivyo hitimisho la kikao na
majumuisho ya Mwenyekiti wa CCM Taifa lilikuwa ni kukemea kwa nguvu zote pirika
hizo na uvunjifu huu wa makusudi wa kanuni za Chama chetu ambazo kimsingi
pirika hizi zinakigawa Chama na kuvuruga mshikamano na umoja ndani ya Chama.
Nasisitiza nukuu hiyo ya baadhi ya
vyombo vya habari si sahihi na ni ya kupotosha ukweli. Inaelekea kuna kikundi cha watu
wanamgombea wao wa kuchonga ambaye bila shaka anapungukiwa na sifa, hivyo
wanajaribu kumuongezea sifa kwa kumlisha Mwenyekiti maneno na kuwaapa baadhi ya
waandishi, uhuni huo haukubaliki.
CCM ina kanuni na taratibu zake
zinazoisimamia na kuiongoza katika kufanya shughuli zake mbalimbali zikiwemo za
mchakato wa kuwapata wagombea wake katika ngazi mbalimbali kuanzia shina hadi
taifa.
Kanuni hizo ni pamoja na kanuni za
Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari,
2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012.
Katika Kanuni za Uchaguzi wa CCM Toleo
la 2012 kanuni za jumla Ibara ya 33 inazungumzia Miiko ya kuzingatiwa wakati wa
shughuli za uteuzi na uchaguzi. nanukuu“ Maadili na nidhamu ya chama katika
kusimamia na kutekeleza shughuli za uchaguzi wa chama lazima kuzingatiwa na
wale wote wanaohusika. Hivyo yawapasa kuelewa na kutambua kuwa;-
(1). “….wanachama wenye
nia ya kugombea hawaruhusiwi kufanya kampeni ya aina yoyote kabla ya majina yao kuteuliwa na kikao
kinachohusika”.
(4). “Ni mwiko kwa
kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya
chama, au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za chini chini kinyume na ratiba
ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa”.
Ibara hiyo ya 33 kifungu kidogo cha
1 na 4 vinaweka wazi msimamo wa kikanuni wa Chama. Hivyo basi kwa mujibu wa
kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la
Februari, 2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012 na kwa mujibu wa
maagizo yaliyotolewa na kupokelewa kwenye kikao cha Mwenyekiti wa CCM Taifa na
wabunge wa CCM mjini Dodoma tarehe 19/05/2013;
Ni marufuku kwa mwanachama yeyote
wa CCM anayetaka kuomba CCM impe nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi wa dola kujipitishapitisha
na kuita wapiga kura na kukutana nao kinyume na kanuni za Chama. Hatua kali
zitachukuliwa kwa mwana CCM yeyote atakaye kiuka agizo hili.
Lakini pia ni marufuku kwa viongozi
na watendaji wa Chama kujihusisha na kuwakusanyia wapiga kura watu hao wenye
nia ya kugombea kupitia CCM kwenye uchaguzi wa dola. Hatua kali zitachukuliwa
dhidi ya viongozi na watendaji wote watakao kiuka agizo hili la Chama.
Tunawataka wote wenye nia, viongozi
na watendaji wa CCM kuzingatia agizo hili, ili tusije laumiana mbele ya safari.
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
NIMETUMIWA NA ADAM MZEE.
1 comments:
Maadili ya chama yapo, maandishi mazuri tu, lkn viongozi ni watu, wana kasoro zao, ....ndio maana kwa jambo lolote kwanza unatakiwa ufundishe `imani' ...ukiamini ndio unaweza ukatenda kwa uthabiti.
Imani haipo, uzalendo haupo, watu wapo kimaslahi zaidi...unafikiri hilo litafanikiwa?
Cheo sio dhamana tena, cheo kimekuwa ni bidhaa, yenye gharama binafsi, ...hatutafika
Post a Comment