Pages

Subscribe:

Ads 468x60px

Wednesday, 18 November 2009

MTUHUMIWA MAUAJI YA RWANDA ASHINDA RUFAA

MAHAKAMA maalumu ya Umoja wa Mataifa UN inayosikiliza kesi za mauaji ya halaiki yaliyotokea mwaka 1994 nchini Rwanda imemwachia huru mtuhumiwa ambaye awali alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 22 jela.

Bw. Protais Zigiranyirazo, ambaye ni mpwa wa Rais wa zamani wa Rwanda, Bw. Juvenal Habyarimana,aliachiwa huru juzi baada ya mwaka jana Mahakama hiyo kumtia hatiani kwa kula njama za mauaji ya watu wapatao 1,000.

Hata hivyo baada ya kukata rufaa majaji wa Mahakama hiyo walisema kuwa kuna makosa makubwa yaliyofanyika katika uendeshaji wa kesi hiyo na ukiukwaji mkubwa wa sheria.

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC ameripoti kuwa baada ya kutolewa maamuzi hayo Bw. Zigiranyirazo alionekana kutoamini kilichotokea huku akipongeza kuhusu uamuzi huo.

"Mungu mkubwa na haki imetendeka, nimefurahi sana," aliiambia BBC.

Ndege iliyokuwa imembeba Rais Habyarimana ilitunguliwa April 6 mwaka 1994, hali ambayo ilisababisha kulipuka mapigano ya siku 100 ambayo yalisababisha vifo vya watu wanaokadiliwa kufikia 800,000 kutoka makabila ya Wahutu na Watutsi.

Katika mapigano hayo, Bw. Zigiranyirazo alikuwa akishutumiwa kuongoza kundi ambalo liliwashambulia Watutsi ambao walikuwa wakitafuta hifadhi milimani siku chache baada ya mauaji hayo kuanza.

Shirika la habari la Uingereza AP limeripoti kuwa hata hivyo jana Jaji Theodor Meron alisema kuwa katika maamuzi hayo kulikuwa na makosa mengi katika uwasilishaji vielelezo.

Baada ya hukumu hiyo Bw. Zigiranyirazo aliiambia BBC kuwa atahitaji kulipwa fidia katika kipindi cha miaka nane na nusu ambayo alikuwa amekwishatumia akiwa kifungoni.

Kwa upande wa Serikali ya Rwanda, Waziri wa Sheria aliiambia BBC kuwa Serikali haikufurahishwa na uamuzi huo lakini akasema kuwa haina uwezo kutengua maamuzi hayo.(BBC)

0 comments: