Friday, 25 February 2011
MAANDAMANO LIBYA: GADDAFI AMTUPIA LAWAMA OSAMA BIN LADEN..!!!
Majeshi yanayomuunga mkono kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi yameshambulia waasi wanaoishikilia baadhi ya miji karibu na mji mkuu wa Tripoli, huku kukiwa hakuna ishara kuwa majeshi hayo yameweza kuvunja msukumo wa wapinzani kupata ushindi.
Akitoa wito wa kusitishwa kwa vurugu, Kanali Gaddafi ametupa lawama kwa kiongozi wa kundi la Al- Qaeda Bw. Osama bin Laden kuhusiana na uasi nchini Libya, akisema maandamano yanayoendelea yanachochewa na watu wanaotoa fedha pamoja na dawa za kulevya.
Katika mji wa Benghazi ambako uasi ulianzia hali watu wamekuwa wakisheherekea ushindi katika mji huo huku wanasesere waliotengenezwa kwa mfano wa Gaddafi pamoja na familia yake wananing’inia katika nguzo za taa za barabarani, na watu wamekuwa wakiimba kauli mbiu na kufyatua risasi hewani.
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Ufaransa anayehusika na masuala ya haki za binadamu amesema kuwa huenda kiasi cha hadi watu 2,000 wameuawa hadi sasa katika vuguvugu hilo ambalo lilianza mnamo Februari 15 mwaka huu.
Wakati huo huo bei ya mafuta ghafi duniani imepanda hadi kufikia dola 120 kwa pipa, ikiwa ni ongezeko kubwa kabisa tangu mwezi Agosti 2008, kabla ya kushuka tena na kufikia karibu zaidi ya dola 111 kwa pipa kutokana na vurugu za Libya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment