Pages

Subscribe:

Ads 468x60px

Tuesday, 31 May 2011

KIKOMBE NDANI YA SINGIDA.HIVI VIKOMBE SASA IMEKUWA KAMA FASHION , KILA KUKICHA WATU WANASEMA WAMEOTESHWA KUTOA TIBA YA VIKOMBE.......

SOMA HABARI HII.
Baadhi ya wagonjwa waliokunywa kikombe kwa Babu wa kijiji cha Samunge wilayani Loliondo ambao hawakupona, wameanza kumiminika kwa mwanafunzi wa kidato cha tatu mkoani Singida Zubeda Nassoro (19) ambaye anadai kuoteshwa kutoa tiba ya kikombe kwa wagonjwa wenye magonjwa sugu.

Zubeda ambaye alikuwa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya kata ya Mungumaji Manispaa ya Singida, hajaenda shule toka Machi 19 mwaka jana baada ya kuanza kuugua magonjwa ya ajabu ajabu.

Amedai hali hiyo ya kuugua ugua, ilipelekea kuoteshwa tiba ya magonjwa sugu ambayo ni magome ya mti wa mwembe, anayodai kutibu magonjwa ya Ukimwi, Kisukari, Kifafa na Kifua Kikuu.

Akizungumza na wananchi Zubeda alisema kati ya wagonjwa 1,200 waliofika kwake kupata kikombe, walimweleza kuwa wamewahi kunywa kikombe kwa Babu mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwasapila lakini hawajapona.

Alipoulizwa kama anayo majina au idadi ya wagonjwa hao na makazi yao yapo wapi, alijibu “Kwa kweli sijaona umuhimu wowote wa kuorodhesha majina ya wagonjwa wanaofika kwangu, wakiwemo waliotoka kwa Babu Loliondo”.

Hata hivyo amesema wagonjwa hao waliopata kikombe Loliondo, wametoka mkoa wa Arusha, Mara na sehemu mbali mbali za mkoa wa Singida, huku idadi ya wagonjwa ikizidi kuongezeka na kufikia wagonjwa kati ya 40 na 50 wanaopata kikombe kila siku.

Zubeda amesema wagonjwa wengi tu wamerudi na kutoa ushuhuda kuwa baada ya kupata kikombe, wameishapona maradhi yaliyokuwa yanawasumbua, japokuwa hao waliotoa ushuhuda huo pia hana idadi yake wala majina yao .

Katika hatua nyingine Zubeda ametumia fursa hiyo kukanusha uvumi ulioenea kuwa amehamisha shughuli zake na kuzipeleka mkoani Arusha.

Amedai kuwa atendelea kutoa tiba kutoka nyumbani kwao hadi hapo atakapojenga kituo maalum hivi karibuni kijijini kwao.

Amenukuliwa akisema “Serikali ya kijiji chetu imekwishanipa eneo la kujenga kituo hicho ambacho kitatumika kutolea tiba na kulaza baadhi ya wagonjwa”.

Aidha, ameiomba serikali wilayani Singida, impatie ulinzi kwa madai kuwa kuna vijana wameanza kufika nyumbani kwao na wana dalili zote za ujambazi.

Kuhusu kuendelea na masomo yake, Zubeda amesema uongozi wa shule ya sekondari ya kata ya Mungumaji, wamemwagiza kwamba ni lazima arudi shuleni Julai mwaka huu bila kukosa.

“Kwa kweli ninavyojiona mimi, sidhani kama ninaweza kuendelea na masomo, nadhani itakuwa ngumu mno, hebu tusubiri kwanza tuone huo mwezi wa saba itakuwaje”,alisema.

Kuhusu dawa yake kufanyiwa utafiti na wataalam kama inafaa kwa matumizi ya binadamu, Zubeda amesema wapo watafiti/wataalam kutoka wilayani ambao walichukua dawa yake kwenda kuifanyia utafiti, lakini hadi sasa majibu ya utafiti huo hayajatolewa.

Zubeda mtoto wa kwanza wa Nassor Hamisi Ghumpi, anatoa tiba ya kikombe kwa gharama ya shilingi 1,100/=, ikiwa shilingi 500/= ni za wahudumu wanaotafuta magome ya mti wa mwembe, 500/= zingine ni ya mtoa huduma na shilingi 100/= inayobaki ndio ya kwake yeye mganga.

0 comments: