Pages

Subscribe:

Ads 468x60px

Tuesday, 13 September 2011

Ajali haina kinga mpaka lini?

TUMEAMBIWA na kukubali kutokana na imani zetu na uzoefu tulioupata katika maisha kuwa ajali haina kinga. Inapotokea ajali imekuwa kawaida kujiliwaza kwa kusema huo ni mtihani na kazi ya Mwenyezi Mungu na kuambizana tuvute subira.

Lakini ni vyema tukakumbuka kwamba tumeambiwa: “Tahadhari kabla ya hatari”. Usemi huu unakusudia kusisitiza umuhimu wa kuchukua hadhari, yaani kinga.

Ajali ni ajali, lakini nyingine siyo tu zinasikitisha, bali zinashtua, kutisha na kuzusha maswali mengi zinapotokea. Hivi sasa nchi yetu imo katika msiba mkubwa baada ya kupinduka na kuzama meli ya Spice katika mkondo wa Nungwi, katikati ya Visiwa vya Unguja na Pemba.

Zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha na waliookolewa, idadi yao kwa mujibu wa taarifa rasmi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ni 619. Hata hivyo, bado kuna idadi kubwa ya watu ambao hawajulikani waliko na inasadikiwa kuwa baadhi yao wamenasa ndani ya meli hiyo.

Taarifa za awali kutoka serikalini zilisema idadi ya abiria waliokuwamo melini ni 600, lakini ukweli uliothibitishwa na taarifa ya SMZ kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed ni kwamba hadi jana, ilikuwa imethibitika ilikuwa na watu 816.

Idadi hii inaweza kuongezeka ikiwa maiti zaidi watapatikana au watu wengine walionusurika kujitokeza. Watu waliookolewa wamesema meli ilisheheni abiria kupita kiasi, mbali ya mzigo mkubwa wa mchele, sukari, magodoro na bidhaa nyingine.

Hili linaonyesha wazi kuwepo kwa uzembe wa aina fulani. Uzembe huu si mwingine, bali ni kitendo cha wahusika kuruhusu meli kuondoka Zanzibar huku ikiwa na abiria wengi na mzigo kubwa kuliko uwezo wake.

Zipo taarifa kwamba abiria walilalamika kwamba meli imesheheni kupita uwezo wake, lakini hawakusikilizwa, kauli zao zilipuuzwa na wahusika hao katika Bandari ya Zanzibar. Hapa inaonyesha kutokuwapo ukaguzi na usimamizi mzuri wa usalama wa abiria katika bandari hiyo.

Yapo maswali ya kujiuliza ambayo pengine Watanzania wanahitaji majibu ya kuridhisha. Inakuwaje meli ya abiria 600 ichukue watu 819? Inakuwaje meli hiyo iwe na maboya 200 yasiyofikia hata robo ya idadi ya abiria waliokuwamo katika meli hiyo?

Huu ni uthibitisho kwamba hata ukaguzi katika meli kubaini usalama wake kwa abiria huwa haufanyiki na kama unafanywa, basi huwa ni kutimiza wajibu tu usio na tija kwa watumiaji wa vyombo hivi vya majini.

Kwa wanaofahamu jinsi vyombo vya usafiri wa majini vinavyofanya kazi kati Zanzibar, Dar es Salaam, Pemba na Tanga wanasema yapo matatizo mengine mengi. Mathalan, wanasema ni kawaida kusikia meli imesimama katika bahari kuu kutokana na kuishiwa mafuta.

Katika hali hii meli au boti hulazimika kutia nanga kwa saa kadhaa zikingojea kupelekewa mafuta kwenye mapipa kutoka katika bandari ambayo huwa karibu zaidi na eneo nanga ilikowekwa.

Mbali na hilo meli hizi hazifuati ratiba na wakati mwingine abiria huwasubiri wana familia wenye meli wafike bandarini hata kama kufanya hivyo ni kuwachelewesha wengine. Maelezo pekee yanayopatikana hapa ni maisha ya watu kutothaminiwa.

Tuonavyo huku ni kutojali au kutothamini maisha ya watumiaji wa vyombo vya majini. Kutokana na hali hiyo, tunaunga mkono hatua za SMZ kama alivyosema Aboud kwamba uchunguzi utafanywa na watakaobainika kuhusika na uzembe huo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ni lazima tubadilike sasa. Hatua za uwajibikaji na za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika kuhusika. Wamiliki wa meli, nahodha na mabaharia wake, maofisa wa bandari na wote walioruhusu meli hiyo kufanya safari ikiwa haina usalama.

Lakini pia tabia hii ya Serikali kusubiri maafa makubwa tena yanayosababisha vifo vya watu wengi kiasi hiki ndipo ichukue hatua, haikubaliki. Hapa Serikali zote mbili, yaani SMZ na Serikali ya Jamhuri ya Muungano haziwezi kukwepa kubeba mzigo.

Ikumbukwe kwamba maisha ya mtu yakishapotea, hayawezi kurejeshwa kwa uchunguzi wala hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wahusika. Tubadilike. Tuache kuoneana muhali na kulindana kwa uzembe.

Lazima uwepo mfumo wa kiutendaji serikalini ambao utaiwezesha kusimamia taasisi zilizo chini yake kama Mamlaka za Bandari na nyinginezo ili kuepusha idadi kubwa ya vifo kama ilivyotokea Tanzania Zanzibar.
Chanzo gazeti la mwananchi.

1 comments:

Yasinta Ngonyani said...

ni swali nzuri mpaka lini ...lakini hii yote unaweza ukasema ni uzembe tu wa serikali kutochunguza kwa makini vyombo hivi. Yaani kwanini iwe hivi ..masikitiko sana. Tutasema mpaka lini Mungu ibariki Afrika wakati ni uzembe tu..samahani jamani