Pages

Subscribe:

Ads 468x60px

Monday 19 July 2010

Madhara unayoweza kupata ukivumilia shida kwa muda mrefu.


BILA shaka wengi tumeambiwa mara nyingi kauli hizi “Vumilia tu ndugu yangu” na tukakubaliana na ushauri huo na kuendelea kunyanyaswa, kuonewa na kuumizwa na mambo mabaya wanayotutendea wenzatu katika maisha, bila kujua kuwa uamuzi wa kuvumilia shida una madhara makubwa kwetu.

Takwimu zinaonesha kuwa wana ndoa na wapenzi wengi wanaishi maisha ya uvumilivu usiohitajika, ambao umezifanya familia nyingi kukumbwa na matatizo, yakiwemo matukio ya watu kuua, kujiua au kuwadhuru wengine.

Kisa kikubwa kinachochangia haya yote ni uvumilivu usiokuwa na sababu ambao watu wamekuwa nao wakiamini kuwa shida na uvumilivu ni vitu vinavyokwenda pamoja kwa wakati wote.

Elimu ya Ufahamu na Nafsi inakataa kanuni ya uvumilivu usiokuwa na sababu kwa vile humfanya mhusika aishi nje ya matakwa yake na hivyo kuathiri mfumo wa akili yake na kuvuruga kinga ya mwili, jambo linaloweza kumsababishia mhusika magonjwa ya moyo au bumbuazi.

Wengi kati ya watu wanaoshambuliwa na magonjwa ya moyo nyakati hizi wanatajwa kusababishwa na msongo wa mawazo unaotokana na msukumo wa lazima wa kimaisha wanaokabiliana nao kwenye ndoa, familia, jamii na maeneo yao ya kazi.

Kama hilo halitoshi, vifo vingi vya ghafla, magonjwa ya kudumu yenye tiba wanayosumbua watu yanaelezwa kuchangiwa na hali ya mtu kukata tamaa ya kuishi itokayo ndani.

Usomapo makala haya unaweza kuyathibitisha kwa kufanya uchunguzi wa kuwatembelea wagonjwa wa muda mrefu na kuwauliza historia za maisha yao, utabaini wamekuwa kwenye uvumilivu wa dhiki.

Niandikapo madhara ya uvumilivu, simaanishi watu wasivumilie shida zao, bali katika kila uvumilivu lazima ziwepo sababu za msingi.
Ikiwa mtu anateswa na mume au mke wake lazima ajiulize ana sababu gani ya kuvumilia, na je sababu hiyo ni ya msingi au anatumikia mateso yatakayomuua hatimaye?

Ikiwa mtu atakuwa anavumilia bila kuwa na sababu za msingi hawezi kukwepa madhara niliyoyataja hapo juu, na bahati mbaya wakati mwingi madhara hutokea bila mhusika kujua chanzo.

Ushahidi wa kauli “nilidondoka tu, nilipopimwa nikaambiwa nina presha” upo mwingi, na watu wamekuwa wakiambiwa “moyo wako umetanuka,” kilichotanua moyo hakijui, kumbe ni msongo wa mawazo uliotokana na uvumilivu wake usiokuwa na sababu.

Kitaalamu sababu ya mtu kuvumilia jambo ndiyo ngao ya madhara, kwani hakuna tatizo mtu kuvumilia maumivu wakati wa kujifungua huku akiamini kuwa baadaye atapata mtoto.

Hii ina maana kuwa, lazima mtu afahamu anavumilia kwa faida gani, atapata nini kuishi na mwanaume mlevi anayesumbua kwa tabia zake za usaliti? Kuna faida gani kuvumilia manyanyaso ya bosi kazini au utapata nini kuishi na ndugu anayekutesa? Je, ni haki kwako kuishi maisha ya utumwa?

Kama hakuna faida za msingi, ukiendelea kung’ang’ania maisha ya mateso kwa madai ya kuvumilia, huwezi kushinda mashambulizi yake, ipo siku usiyoijua utajikuta umepata tatizo baya litakalokuweka pabaya zaidi, ambapo hutaweza kupavumilia hata kidogo.

Nimalizie kwa kuweka wazi lengo langu la kuacha uvumilivu usiokuwa na sababu kwa kumtaka kila mtu mwenye shida awe na sababu ya kuivumilia. “Nitavumilia mateso haya, baada ya mwaka mmoja nitamaliza shule na kupata cheti kitakachonisaidia kwenye maisha yangu.” “Nitavumilia mpaka nipate kazi nyingine.”

Nia yangu ni kumfanya kila mvumilivu kuwa na sababu za msingi, wasiokuwa nazo ni bora wakaondokana na uvumilivu wao na kutafuta maisha mengine mbali na hapo wanapopavumilia.
Source Globalpublishers.

5 comments:

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Yawezekana ni kweli. Umesema wewe sijui itakuwaje!

Fulani alisema akaambiwa ameasi dini yake...lol!

Ngoja nsikilizie kwanza :-)

Yasinta Ngonyani said...

Habari hii imenigusa sana, kwani ni kweli kabisa kuna wanawake wanavumilia huku wakipata mateso yaaani basi tu. Nashindwa hata kuendelea kuandika. Ahasnte Edna kwa mada hii.

Anonymous said...

Ni kweli kabisa wanawake wengi hasa wa kitanzania wanapata maradhi ya moyo ukiluza sababu anavumila kwa sababu ya watoto.Wanawake amkeni hii sio karne ya kunyanyasika.

EDWIN NDAKI (EDO) said...

uchambuzi umekaa vema..big u..Nimependa blog yako

EDNA said...

Edwin Asante na karibu sana.